Jumanne , 17th Jul , 2018

Timu ya Wanawake ya Tanzania bara “Kilimanjaro Queens” ambayo imetua alfajiri ya leo jijini Kigali nchini Rwanda, imefanya mazoezi kujiandaa na mashindano ya CECAFA kwa Wanawake yanayoanza Julai 19,2018 nchini humo.

Kilimanjaro Queens wakiwa kwenye uwanja wa Mumena Nyamirambo Rwanda.

Baada ya timu hiyo kufanya mazoezi nchini Rwanda kwa mara ya kwanza, kocha wa timu hiyo Bakari Shime ameeleza kuridhishwa na hali ya wachezaji wake.

''Wachezaji wote wameshiriki kikamilifu katika mazoezi  tuliyofanya leo kwenye uwanja wa Mumena hapa Nyamirambo na kwakweli yametupa matumaini ya kurejea na ubingwa wa CECAFA mwaka huu'', amesema Shime.

Aidha Shime ameongeza kuwa yeye na wenzake kwenye benchi la ufundi ambao ni Kocha msaidizi Edina Lema, Kocha wa makipa Eliuter Mollel, Daktari Blandina Mnambya na meneja wa vifaa Ester Chabruma wanaamini kila walichokifanya kabla, kinatosha kuwafanya wafanye vizuri kwenye michuano hiyo.

Kilimanjaro Queens inayoundwa na wachezaji 20, inatarajia kucheza mchezo wake wa kwanza kwenye mashindano hayo ya CECAFA dhidi ya wenyeji Rwanda Alhamis Julai 19.