KMC kutolewa chambo na Simba, Yanga, Azam FC

Ijumaa , 23rd Aug , 2019

Kuanzia leo Ijumaa hadi Jumapili ya wiki hii, mashabiki wa soka Tanzania wana kazi moja tuu ya kuhakikisha timu nne zinafuzu katika hatua ya pili ya michuano ya vilabu barani Afrika.

Wachezaji, makocha na viongozi wa KMC

Leo KMC itashuka dimbani kucheza mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho dhidi ya AS Kigali katika uwanja wa taifa, ambapo katika mchezo wa kwanza mjini Kigali, timu hizo zilitoka sare ya kutofungana bao lolote.

Katika msimu wake wa kwanza katika Ligi Kuu Tanzania Bara, KMC imefanikiwa kucheza michuano mikubwa barani Afrika huku ikifanikiwa kupata udhamini mkubwa wa Shilingi Bilioni moja, ambao ni historia kwa klabu hiyo.

Pia kesho Jumamosi, Azam FC itawakaribisha Fasil Kenema katika uwanja wake wa Chamazi Complex baada ya mchezo wa awali nchini Ethiopia kumalizika kwa Azam Fc kupoteza kwa bao 1-0. Yanga itakuwa ugenini nchini Botswana dhidi ya Township Rollers ambapo katika mchezo wa awali, timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1.

Simba itawakaribisha UD Songo, Jumapili ya Agosti 25 katika uwanja wa taifa baada ya mchezo wa awali nchini Msumbiji kumalizika kwa sare ya kutofungana.

Akizungumza kuelekea mchezo huo,  Mwenyekiti wa Bodi ya KMC, Benjamin Sitta amesema, "kuna kazi kubwa ya kufanya kwa KMC ila jambo la kwanza ni matokeo kisha mengine yatafuata, wachezaji wanajua wameahidiwa kitu gani, ni jambo la kusubiri".