Jumanne , 22nd Mei , 2018

Kocha wa Mbao FC Novatus Fulgence, aliyechukua mikoba ya Etienne Ndayiragije katikati ya mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara, amesema msimu ujao wataanza maandalizi mapema kukwepa hatari ya kushuka daraja.

Fulgence ameyasema hayo kuelekea mchezo wa leo ligi kuu ya soka Tanzania bara dhidi ya Yanga, ambapo ameeleza kuwa tatizo la timu yake kuwa hadi sasa inapigia kujikwamua kutoshuka daraja ni kutokana na kuchelewa kuanza maandalizi.

''Kama kocha jukumu langu ni kuhakikisha timu inafanya maandalizi mapema ili kujiweka vizuri msimu ujao ikiwemo kusajili mapema maana hapo ndio huwa kuna tatizo kubwa na timu nyingi zinapitia na kujikuta zikipigania kushuka daraja'', amesema.

Kuhusu mchezo wa leo Fulgence amesema ni mchezo muhimu kwani wakishinda utawasaidia kuhakikisha wanakwepa janga la kushuka daraja msimu huu ambao ni wa pili kwao kwenye ligi kuu.

Mbao FC imekutana na Yanga mara tatu katika michezo ya ligi na haijawahi kufungwa hata mchezo mmoja. Katika mchezo wa raundi ya kwanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-0. Mabao hayo yalifungwa na mshambuliaji Habibu Kiyombo.