Ijumaa , 10th Jul , 2020

Kocha msaidizi wa klabu ya Tanzania Shaaban Kazumba amesema kitendo cha wao kufungwa na Coastal Union ya Tanga kwa bao 2-1 katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara,sasa anaanza kuamini kwamba masuala ya kishirikina yanaweza husika katika mpira wa miguu.

Kikosi cha Tanzania Prisons katika picha ya pamoja kwenye moja ya mchezo wa ligi kuu kandanda Tanzania bara.

Kazumba maarufu kwa jina la Mourinho amesema alishangazwa na  matokeo ya mchezo wa jana kwa kuwa walitawala kwa asilimia kubwa mchezo huo lakini ajabu wao ndio waliofungwa kwa mabao ya kushtukiza.

Kocha huyo ameongeza kuwa, wachezaji wa Coastal Union ni wajanja na wanajua kutumia maarifa ndio maana waliwapiku na kufunga mabao yaliyowekwa kimiani na Shaaban Hammis na Kanduru Hamis lakini Prison ilipata bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penati uliofungwa na Cleofas Mkandara.

Hata hivyo Kazumba amesema baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Coastal Union nyumbani, sasa wanajiandaa na mechi zijazo tatu za ugenini dhidi ya Ndanda, KMC na Namungo ili kujua nafasi watakayomaliza msimu huu.

Kipigo cha jana ni cha kwanza kwa Prisons kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, na wanasalia katika nafasi ya 10 wakiwa na alama zao 44,huku ushindi kwa Coastal Union ukiwaimarisha katika nafasi yao ya 5 wakiwa na alama 51.

Tangu kurejea kwa michezo ya ligi kuu baada ya mapumziko ya dharula kutokana na janga la Corona, Prisons haijapata ushindi katika mechi 5 za mwisho baada ya kutoka sare michezo minne,wakati Coastal Union jana ilipata ushindi wa kwanza jana baada ya kufungwa katika mechi tatu mfululizo.