Jumapili , 22nd Mar , 2020

Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga, Luc Eymael amesema kuwa klabu yake haina nafasi ya kunyakua taji la ligi kuu kutokana na nafasi iliyopo katika msimamo na pointi ambazo imeachwa na Simba.

Kocha Luc Eymael na mashabiki wa Yanga

Luc Eymael amesema kuwa  kwa sasa ni lazima aseme ukweli kwamba kikosi chake hakina uwezo wa kutwaa Kombe la Ligi Kuu Bara kutokana na kuachwa pointi nyingi na Simba.

"Muda mwingine ni lazima niseme ukweli ukitazama mahali nilipo na wapinzani wangu walipo ni mbali hivyo kazi yangu kubwa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji ili wakati ujao sasa wawe na nguvu ya kulisaka kombe ila kwa sasa tusubiri na tuone itakuaje," amesema Eymael.

"Ukiwa kocha wakati mwingine unakuwa kwenye hali ambayo hakuna anayeweza kukuelewa kile ambacho utasema kwa mfano muda huu nikisema sina uwezo wa kutwaa kombe wengi wanaweza wakadhani nimekata tamaa hapana", ameongeza.

Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 71 baada ya kucheza mechi 28 huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu na pointi 51 ikiwa imecheza mechi 27. Yanga ikizidiwa kwa jumla ya pointi 20 na Simba ambao ni mabingwa watetezi.

Ligi imesimama kwa muda wa mwezi mmoja ili kupisha hali kutulia kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona yanayosambaa duniani.