Jumatano , 20th Feb , 2019

Baada ya kumalizika kwa mchezo wa jana, Jumanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya African Lyon na Simba, Kocha wa African Lyon, Suleyman Jabir amesema kuwa Simba ilibebwa kupata matokeo.

Kikosi cha Simba

Katika mchezo huo uliopigwa katika dimba la Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, imeshuhudiwa Simba ikiitandika African Lyon kwa mabao 3-0, ambapo baada ya kocha Jabir kulalamikia maamuzi ya uwanjani, Afisa Habari wa Simba, Haji Manara akaibuka na kujibu tuhuma hizo.

Manara amesema, "hayo maneno ya kubebwa ni ya kawaida, hata Yanga walisema, kila timu inasema, basi tufanye kila timu iwe inakuja na makocha wake na madaktari wake ndio wawe waamuzi kwasababu hizi lugha za kihuni".

"Tatizo la watu wanaaminishana mambo ya kubebwa bebwa, Simba ina uwezo wa kimpira kuliko klabu yoyote Tanzania kwahiyo yoyote atakayekuja ataona anaonewa tu. Kwa 'level' ya Tanzania sisi ni Alpha na Omega", ameongeza Manara.

Baada ya mchezo huo sasa Simba inarejea Jijini Dar es salaam kwaajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya 'Wana lambalamba' Azam FC utakaopigwa Ijumaa, Februari 22.
 

Tazama hapa chini wakijibizana kuhusu tuhuma hizo.