Luc Eymael amtaja Niyonzima ni tatizo Yanga

Jumapili , 16th Feb , 2020

Kocha wa Yanga, Luc Eymael amesema kuwa kutokuwepo kwa kiungo wake muhimu Haruna Niyonzima ndiyo sababu kubwa iliyopelekea kutopata matokeo katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons jana Jumapili.

Kocha Luc Eymael na Haruna Niyonzima

Eymael amesema hayo akizungumza na wanahabari baada ya kumalizika kwa mchezo huo, ambapo amesema kuwa wanapaswa kujilaumu wenyewe kutoshinda mchezo kutokana na kushindwa kutumia nafasi.

"Tulipata nafasi mbili tatu tukashindwa kuzitumia pamoja na penalti ya Morrison ambayo pia alikosa. Mwamuzi wa pembeni alifanya uamuzi wa haki kumshauri mwamuzi wa kati kuwa ni penalti, kwahiyo nampongeza kwa hilo wala sina tatizo naye, ila tatizo lilikuwa kwetu wenyewe", amesema Eymael.

"Katika kiungo tulimkosa Haruna Niyonzima ambaye ndiye anaichezesha timu baada ya kuugua Malaria lakini Alfajiri tutasafiri naye kuwafuata Polisi Tanzania. Niyonzima ana utulivu, ana akili na jicho la mpira awapo uwanjani na hicho ni kitu muhimu sana kwa mchezaji", ameongeza.

Baada ya matokeo hayo sasa Yanga inafikisha pointi 39 katina nafasi ya tatu huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Azam FC ambayo imepoteza kwa kufungwa mabao 2-1 na Coastal Union na kusalia na alama zao 44, wakati huo huo Simba ikiwa kileleni kwa pointi 56 baada ya jana kuifunga Lipuli FC bao 1-0 mjini Iringa.