Ijumaa , 26th Jul , 2019

Mchezo wa ngumi ni miongoni mwa michezo inayopendwa zaidi duniani, haswa kutokana namna inavyoweza kutengeneza majina makubwa kama ilivyowahi kuwa kwa mabondia Muhammad Ali na Mike Tyson ambao walijijengea heshima duniani kote.

Kushoto ni bondia Maxim Dadashev na kulia ni bondia Hugo Santillan.

Wiki hii imekuwa si nzuri kwa mchezo huo kutokana na mabondia wawili kupoteza maisha baada ya kuumia wakiwa ulingoni.

Bondia Maxim Dadashev mwenye miaka 28, raia wa Urusi amefariki Jumanne Julai 23, 2019, ikiwa ni siku 4 zimepita baada ya kutoka ulingoni alikokuwa akipigana na Subriel Matias kwenye pambano la (IBF) Junior welterweight Ijumaa Julai 19 huko Maryland.

Kuna video zinaonesha jinsi mkufunzi wa Dadashev akimsisitiza bondia huyo wasitishe pambano kwani alikuwa na hali mbaya ikiwemo mwili kuchemka kupita kiasi.

Imeelezwa kuwa Dadashev alikuwa na tatizo kwenye ubongo lililotokana na kupigwa ngumi katika mapambano yake mbalimbali yaliyopita pamoja na hilo la Ijumaa.

Bondia mwingine ambaye amefariki wiki hii ni Hugo Santillan mwenye miaka 23 raia wa Argentina, ambaye amefariki baada ya kupigwa na kupoteza fahamu katika pambano dhidi ya Eduardo Abreu wa Uruguay.

Santillan alikimbizwa hospitali na kufanyiwa upasuaji wa ubongo na kinga ya mwili lakini amefariki siku 5 baada ya pambano hilo.

Santillan na Eduardo Javier  walipigana Jumatano usiku huko Buenos Aires Argentina, kwenye pambano la Super lightweight.