Jumanne , 16th Oct , 2018

Timu ya taifa ya Madagascar imeweka historia ya kuwa timu ya pili kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika AFCON mwakani nchini Cameroon baada ya wenyeji wa michuano.

Timu ya taifa ya Madagascar

Historia hiyo imewekwa baada ya kushinda mchezao wake wa nne katika kundi A kwa bao 1-0 dhidi ya Equatorial Guinea katika uwanja wake wa nyumbani, bao lililofungwa na Njiva Rakotoharimalala katika dakika ya 43 ya mchezo huo.

Madagascar pia imeweka historia nyingine ya kufuzu michuano ya AFCON kwa mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipoanzishwa mwaka 1957.

Imefuzu ikiwa na alama 10 baada ya kushuka dimbani michezo minne, nafasi ya pili ikishikiliwa na timu ya taifa ya Senegal yenye alama saba.

Equitorial Guinea ina  alama tatu mpaka sasa baada ya kucheza michezo minne na Sudan ikiburuza mkia baada ya kufungwa michezo yote mitatu iliyocheza.