Madeni mawili wanayotakiwa Simba kulipa kwa Yanga

Jumanne , 6th Aug , 2019

Leo ni siku ambayo mashabiki wa Simba wanajigamba kila kona kuwa wataonesha ukubwa wao katika kilele cha tamasha la 'Simba Day' litakalofanyika katika uwanja wa taifa.

Simba na Yanga

Hii ni kufuatia tamasha la watani wao wa jadi Yanga maarufu kama 'Wiki ya Mwananchi' kuhitimishwa, Agosti 4 kwa ufanisi mkubwa pamoja na mchezo dhidi ya Kariobangi Sharks na kutoka sare ya bao 1-1.

Mashabiki wa Simba wakiongozwa na Msemaji wao, Haji Manara wana deni la kulipa kwa Yanga hii leo kwa kuujaza uwanja, kwani waliwacheka Yanga wakisema kuwa licha ya kujaa uwanjani lakini bado kulikuwa na mapengo mengi yaliyoonekana.

Deni la pili kubwa ni la matokeo uwanjani, ambapo katika mchezo wa Yanga na Kariobangi, mashabiki wa Simba walikuwa upande wa Kariobangi na wakionekana kuponda kiwango cha Yanga. Leo hii ni zamu yao wakihitaji kupata ushindi ili kusawazisha mambo.

Simba itacheza na Power Dynamos ya Zambia jioni ya leo. Kuelekea mchezo huo, Haji Manara amesema kuwa mashabiki watarajie mambo mengi ya kushangaza uwanjani, ikiwa ni pamoja na utambulisho wa mchezaji mmoja mpya na wa mwisho.

Pia amejigamba kuwa wao Simba ndiyo waanzilishi wa tukio hilo kwa vilabu hapa nchini kwahiyo wanataka kulifanya kwa namna nyingine. Tusubiri kuona kama Simba wataweza kujibu maswali hayo makubwa mawili hii leo.