Jumapili , 17th Feb , 2019

Baada ya kumalizika kwa mchezo wa watani wa jadi Yanga na Simba katika uwanja wa taifa, Shabiki maarufu wa Yanga, Jimmy amezua gumzo mtandaoni baada ya kutoa chozi hadharani kufuatia kichapo cha bao 1-0 ilichokipata timu yake.

Haji Manara na Jimmy akiwa na mkewe (kulia)

Jimmy ambaye mara kwa mara hushiriki katika kipindi cha Kipenga Extra cha East Africa Radio, alimwaga chozi mbele ya waandishi wa habari akisema kuwa anahofia zaidi juu ya ahadi ambazo aliziahidi kwa wapinzani wake Simba katika mchezo huo.

Aliahidi kuwa endapo Yanga ikifungwa na Simba, atamweka rehani mkewe na yeye mwenyewe kuvua nguo Kariakoo, ambapo alikuwa akiwaomba mashabiki wa Simba wamsamehe kwa ahadi zake.

Suala hilo limemuibua Afisa Habari wa Simba, Haji Manara ambaye katika ukuirasa wake wa Instagram ameandika, "ninakuombea msamaha ili mkeo anusurike!!. Simba ni watu waungwana na kwa kuwa umeomba radhi tunaamini uliyepinga nae atakusamehe pia, ila 'next time' iwe fundisho kwa wafuasi wa Mbuteni msithubutu kutoa ahadi kwa bingwa wa nchi,!".

Baada ya kutoka uwanjani na kufika nyumbani kwake, hali ya Jimmy haikuwa nzuri kwani alikuwa akilalamika mbele ya wazazi na ndugu zake lakini akishindwa kueleza nini kinamsumbua.

Katika ukurasa wa Istagram wa George David 'Kampista' ambaye ni mtangazaji wa michezo East Africa Radio, ameweka video inayoonesha hali ya shabiki huyo baada ya kufika nyumbani kwake.