Jumapili , 21st Apr , 2019

Kufuatia kufungwa dhidi ya Kagera Sugar katika ligi, Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amemtaka kocha wa Yanga kujifunza jinsi ya kuzungumza pindi timu yake inapofungwa.

Haji Manara na Mwinyi Zahera

Kupitia ukurasa wake wa Istagram, Manara ameanza kwa kumsifia kocha wake, Patrick Aussems kwa kitendo cha kuwapongeza wapinzani wake Kagera Sugar kutokana na kiwango walichokionesha dhidi yao, huku akimtaka kocha wa Yanga Mwinyi Zahera kuiga mfano huo badala ya kulalamika kuwa wanaonewa.

Manara ameandika, "tofauti ya kocha wa mpira na kocha wa Sunsumia au kibao kata!!. Unafungwa unawapongeza washindi na kukubali mapungufu yako, angekuwa yeye sasa!, "waamuzi wanatuonea, mimi nimefundisha Ulaya miaka arobaini", ( ukigoogle ) huoni timu alizofundisha zaidi ya kufundisha kucheza ndombolo na mayenu ). "Ohh Simba inabebwa, leo sikushinda kisa Ajibu na Fei Toto hawakuvaa boksa na hawajala toka juzi!!".

"Hahahahaha ila akishinda sasa, najua kupiga gitaa kuliko Diblo, na ile fasi ya putuluu imekuja na ndege na ndio maana sisi Wakongo tunapendwa na wadada wa bongo. Kocha mzuri huzungumzia vitu 'technical' na sio riwaya za wanaotumia mkorogo wa buku buku!!!", ameongeza Manara.

Baada ya kupoteza mchezo huo, sasa Simba inasalia na pointi zake 60 baada ya kucheza michezo 24, huku Kagera Sugar ikiwa katika nafasi ya 13 na pointi 39 baada ya kucheza mechi 33 mpaka sasa. 

Baada ya mchezo huo, Simba inaendelea na ratiba ya kupunguza viporo vyake ambapo sasa inajiandaa kucheza na Alliance FC jijini Mwanza, April 23 katika dimba la CCM Kirumba.