Manara ataka kombe likabidhiwe kwa Rais Magufuli

Jumatatu , 18th Mei , 2020

Afisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara amesema endapo Simba itabeba ubingwa wa ligi ataongea na uongozi wa klabu ili ikiwezekana kombe hilo wamkabidhi Rais Magufuli.

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara

Amesema hayo kufuatia hotuba ya Rais Magufuli jana, Jumapili kwamba ataangalia mwenendo wa ugonjwa wa COVID-19 nchini katika wiki hii ili kuona kama anaweza kuruhusu vyuo kufunguliwa na shughuli za michezo kuendelea.

Manara amesema kuwa Simba imebakiza muda mchache sana kushinda ubingwa, hivyo haimaanishi kwamba wasichukue tahadhari pindi ligi itakaporejea, "kutokana na taarifa hii ya Mhe. Rais, mashabiki wa Simba nawaomba musipuuze tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona hata kidogo, tusimwangushe Rais wetu, ameruhusu hili jambo kwahiyo ikirejea tuchukue tahadhari".

"Kwakuwa Rais ndiye aliyeagiza ligi irudi, hatuna ubaya wala si dhambi tukimpelekea Mhe.Rais ikimpendeza akae nalo, ikibidi likae Ikulu kwa sababu hii itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kuchukua. Sisi tuna makombe 53 kabatini kwetu, tukimpa hili hatutapungukiwa na kitu", ameongeza Manara.

Kwa upande wa Bodi ya Ligi Kuu nchini Tanzania (TPBL) imesema kuwa ina nia ya kumaliza msimu wa ligi kwa kucheza michezo yote iliyosalia na kinachosubiriwa ni ruhusa ya Serikali ili maandalizi yaanze kufanyika.