Ijumaa , 22nd Mar , 2019

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amezungumzia sababu ya uwepo wa wanadada maarufu nchini, Hamisa Mobetto na Wema Sepetu katika kamati ya kuhamasisha ushindi wa Taifa Stars dhidi ya Uganda.

Haji Manara, Hamisa Mobetto na Wema Sepetu

Kuelekea mtanange huo wa kufa na kupona wa kuwania kufuzu michuano ya AFCON kati ya Taifa Stars na Uganda utakaopigwa katika Uwanja wa Taifa, Manara amejibu maneno ya watu wanaohoji kuhusu uwepo wa wanadada hao kwenye kamati ilhali hawana uelewa wowote wa soka nchini.

Kupitia mtandao wa Instagram, Manara amesema, "wengine wanahoji hivi Kwenye kamati ya team ya Taifa, kina Wema Sepetu na Hamisa Mobetto wanafanya nini?. Hebu tuweni 'serious' kidogo guys!!".

"Hawa wapo katika kamati ya hamasa ya timu ya taifa, na wapo watu wengi wenye ushawishiwi na kamati hii ya hamasa ipo chini yangu ikiwa chini ya kamati ya ushindi ya timu ya taifa iliyopo chini ya RC Makonda, ambapo mimi ni mjumbe. Guys hivi hamuoni hiyo kazi wanayofanya hawa wasanii na watu maarufu katika kuitangaza mechi hii ya Jumapili?. Nani leo hajui kuwa Jumapili kuna Mtanange wa kufa mtu Taifa?", amemalizia Manara katika ujumbe wake.

Kamati hiyo ya kuhamasisha Taifa Stars ilifanya mkutano wake na wanahabari jana Jijini Dar es salaam, ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda. Pamoja na mambo mengine, mkuu huyo wa mkoa alimtangaza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi wa mtanange huo.

Taifa Stars inahitaji ushindi katika mchezo dhidi ya Uganda ili iweze kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwezi June, 2019 nchini Misri. Mara ya mwisho kwa Taifa Stars kushiriki michuano ya AFCON ni mwaka 1980 nchini Nigeria.

Bonyeza hapa chini kutazama zaidi.