Jumatano , 20th Feb , 2019

Msemaji wa Klabu ya Mabingwa watetezi, Simba, Haji Manara amesema kwamba anaamini miaka kumi ijayo asilimia 90 ya watanzania watakuwa mashabiki wa klabu hiyo.

Haji Manara

Manara ameyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa African Lyon na Simba uliopigwa jana katika uwanja wa Sheikh Ari Abeid Jijini Arusha.

"Nimefanya nini katika Taifa hili?, Mimi sio msanii, sio bondia, sio mwanamuziki na sio lolote!!...Ahhh kuna kitu Mungu ananiambia na kwangu nitaendelea kuwashukuru sana Simba kunipa fursa niliyoitumia vema kwa interest ya klabu na pia kwangu kutengeneza brand isiyogusika Tanzania.

Ameongeza, "Yes, naamini baada ya 'Ten Years over' 90 % ya watu wa Taifa hili wote watakuwa mashabiki wa kulia wa Simba".

Furaha ya Manara siku ya jana ilianza baada ya kutembelea shule ya msingi jijini humo na kupokelewa wa shangwe huku baadae Kapteni wa Simba, John Bocco na Adam Salamba wakiinogesha kwa kubeba poiti tatu muhimu ambapo zimefanya sasa Simba kuwa na jumla ya pointi 42.

Katika msimamo wa ligi mpaka sasa Yanga inaongoza ikiwa imeshacheza michezo 24 na kujikusanyia pointi 58, Azam FC inashika nafasi ya pili kwa pointi 50 baada ya kushuka dimbani michezo 24 huku Simba yenyewe ikiwa imecheza michezo 17 na kubeba pointi 42 katika nafasi ya tatu.