Jumamosi , 21st Jul , 2018

Kufuatia maamuzi ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA kuipiga faini nyingine klabu ya AS Roma kutokana na vurugu za mashabiki na kauli tata za viongozi katika msimu wa ligi ya mabingwa Ulaya uliomalizika, tunatazama jinsi viongozi na mashabiki hao walivyoigharimu klabu yao.

Mashabiki wa AS Roma wakiisapoti timu yao katika moja ya mchezo

Mmiliki wa wa klabu ya AS Roma ya nchini Italia, James Pallotta amefungiwa miezi mitatu kuhudhuria michezo yoyote ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA kuanzia sasa kwa kosa la kumdharau mwamuzi.

Pallotta amepewa adhabu hiyo kufuatia kauli yake ya kumwita mwamuzi ‘kituko’ katika mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya kati ya AS Roma na Liverpool uliofanyika Mei, 2 mjini Roma ambapo klabu yake licha ya ushindi wa 4-2, iliondolewa katika hatua ya nusu fainali.

Katika maamuzi hayo yaliyotelewa na UEFA, pia klabu ya AS Roma imepigwa faini ya Euro 19,000 ambazo ni sawa na takribani shillingi millioni 50.4 za kitanzania kutokana na vurugu za mashabiki .

Katika mchezo wa awali wa nusu fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, AS Roma ilipigwa faini ya Euro 50,000 ambazo ni sawa na takribani shillingi millioni 132.6 za kitanzania kutokana na vurugu za mashabiki ambazo zilipelekea kujeruhiwa vibaya kwa shabiki mmoja wa Liverpool.

Kwenye msimu uliopita wa ligi ya mabingwa barani Ulaya, klabu ya AS Roma imetozwa jumla ya Euro 89,000 ambazo ni sawa na takribani shilling za kitanzania millioni 236.1 kutokana na vurugu za mashabiki na kauli tata za viongozi wa klabu hiyo.