Jumamosi , 23rd Jan , 2016

Wanachama wa klabu ya Coastal Union ya jijini Tanga wameutaka uongozi wa timu hiyo kujiuzulu kwa kuwa wameshindwa kuiendesha timu kutokana na matokeo mabaya katika michuano ya ligi kuu ya Soka Tanzania Bara.

Abdul Famau ambaye ni mmoja wa wanachama wa klabu hiyo ambaye amesema kwamba matatizo yanayoikumba timu hiyo ni mengi ikiwemo wachezaji kucheleweshewa mishahara pamoja na kambi duni.

Famau amesema, matatizo yote yanayoikumba klabu yao yamesababishwa na mkurugenzi wa hadhi na sheria wa Shirikisho la Soka nchini TFF Eliud Peter Mvela kwani ndiye aliyeuvuruga uchaguzi mkuu wa klabu yao kwa maslahi ya kikundi cha watu.

Kwa upande wake afisa habari wa Coastal Union Oscar Assenga msemaji wa timu hiyo yeye kwa upande wake amesema matokeo mabovu yanawaumiza hata wao viongozi hivyo amewaomba wanachama wa timu hiyo kushikamana ili kuinusuru timu yao.

Assenga amesema, matokeo katika timu hayaji kwa mara moja, na kinachotakiwa ni wanachama kushikamana ikiwa ni pamoja na kuipa timu yao sapoti ili iweze kufanya vizuri katika michezo mbalimbali ya ligi kuu pamoja na Kombe la Shirkisho.