Jumanne , 17th Jul , 2018

Mlinda mlango mkongwe nchini Juma Kaseja ambaye amesajiliwa na klabu ya KMC ya Kindondoni, ametoa mtazamo wake juu ya suala la TFF kuruhusu timu za ligi kuu kusajili na kuwatumia wachezaji 10 wa kigeni kwenye mchezo mmoja akisema suala hilo waachiwe mashabiki. 

Mashabiki wa Yanga na Simba kwenye moja ya mechi zilipokutana timu hizo.

Ameeleza kwa upande wake na kiufundi zaidi anaichukulia kama ni changamoto tu kwa wachezaji wazawa lakini kwa upande wa mashabiki wao ni lazima wafurahie endapo timu yao ina uwezo wa kusajili hao wachezaji wa kigeni na maumivu kwa wale ambao timu zao hazina uwezo huo.

“Kuongeza wachezaji 10 ni jambo ambalo limekaa katika pande mbili, kiufundi ni changamoto nzuri kwa wachezaji wa ndani na linazisaidia baadhi ya timu zenye uwezo wa kufanya hivyo. Upande mwingine ni mbaya kwa baadhi ya timu zisizo na uwezo wa kusajili hao wachezaji lakini sisi wachezaji tusilalamike hilo tuwaachie mashabiki sisi tufanye kazi yetu ya kucheza'', - amesema.

Katika kutaka kujua athari kwa timu ya taifa tumemtafuta aliyekuwa kocha wa timu ya taifa, Salum Mayanga bila mafanikio, lakini tumempata kocha wa makipa wa Azam FC Iddy Abubakary, ambaye amesema wachezaji wa Tanzania wanatakiwa waitumie hii kama elimu na wakifanya hivyo watajituma zaidi na kwenda kucheza soka nje na timu ya taifa itafanya vizuri.

Mlinda mlango Juma Kaseja

“Tutasimama palepale kwamba wachezaji wetu wakitanzania wanatakiwa waliangalie jambo hili kwa umakini. Kama mchezaji anatoka Kenya au Uganda anakuja kucheza hapa basi na wao wanaweza kwahiyo wajitume watoke nje ili wakirudi timu yetu ya taifa ipate wachezaji wazuri'', amesema Iddy.

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania(TFF), imefanya mabadiliko hayo ya kutoka wachezaji 7 hadi 10 kwa kile ilichoeleza ni kuongeza ushindani na kuifanya ligi iwe na changamoto kutokana mataifa tofauti itakayowafanya wachezaji wa ndani wawe na viwango bora.