Jumapili , 20th Sep , 2020

Afisa Habari na Msemaji wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema hayupo tayari kuongelea kuhusu masuala ya Yanga kwa sasa ikiwa kauli hiyo haipo kwenye tovuti 'website' pamoja na mitandao yao ya kijamii.

Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli

Kauli hiyo ameitoa hii leo alipozungumza na EATV na Radio Digital kwa njia ya simu kutaka kufahamu tathmini ya mauzo na hali ya usambazaji wa jezi mpya za klabu hiyo zilizozinduliwa Ijumaa iliyopita ikiambatana na ufunguzi wa duka jipya ya vifaa vya michezo mali ya timu hiyo makao makuu ya timu, Kariakoo mtaa wa Twiga na Jangwani.

Sio lazima tuweke kila kitu kule, ukiona hakipo kule ujue hatupo tayari kukisemea. Sio kila kampuni inapofanya kila jambo liwekwe hadharani, niulize yale ambayo uliyoyaona kwenye website na mitandao yetu ya kijamii, usipoyaona usiniulize maana hatupo tayari kuyasemea”, amesema Bumbuli.

Itakumbukwa kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wapenzi na wadau wa timu ya Yanga hususani wale wa mikoani wakilalamikia ulanguzi wa jezi hizo hadi kufikia zaidi ya shilingi elfu 70,000 za kitanzania ambapo ni tofauti na bei elekezi shilingi za kitanzania 35,000 kutoka kwa wasambazaji na wauzaji wakuu kampuni ya GSM.

Mauzo ya jezi hizo yameelezwa kuwa ni makubwa hii ni kufuatiwa thamani ya timu hiyo kuongezeka kupitia usajili wa wachezaji wenye majina na viwango vikubwa barani Afrika akiwemo Sergie Mukoko na Tuisila Kisinda kutoka DRC Congo, Carlso Carmo Carlinhos kutoka Angola, Michael Sarpong kutoka Ghana, Yacouba Songne kutoka Ivory Coast, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya, Farid Mussa na wachezaji wengine wazawa.