Mazoea yaziponza Yanga na Simba

Jumatatu , 11th Mar , 2019

Shirikisho la soka nchini (TFF), limeashusha rungu kali kwa vilabu vikongwe nchini vya Simba na Yanga baada ya timu hizo kukiuka kanuni za mpira wa miguu kwa kutenda makosa kadhaa kwenye ligi kuu.

Simba na Yanga

Akiongea leo kwenye makao makuu ya TFF, Afisa habari wa shirikisho hilo, Cliford Ndimbo amesema kamati ya saa 72, imepitia makosa mbalimbali ya timu za ligi kuu ikiwemo Simba na Yanga hivyo kutoa adhabu kwa mujibu wa kanuni.

Mabingwa watetezi Simba na vinara wa ligi msimu huu Yanga wametozwa faini ya jumla ya shilingi milioni 9, kwa kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanja wa taifa kwenye mchezo wa watani hao wa jadi Februari 16, 2019.

Yanga ambayo ilijikusanyia jumla ya milioni 165,215,792.86 kwenye mchezo huo imepigwa faini ya shilingi milioni 9 wakati Simba wakitozwa shilingi milioni 3.

Mbali na hilo Yanga imepata pigo kwenye eneo lake la ulinzi baada ya Kamati ya Nidhamu ya TFF, kumtia hatiani mchezaji Abdallah Shaibu kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Coastal Union na kamati kumfungia mechi tatu mfululizo/zinazofuatana kwa mujibu wa kifungu cha 48(1)(d) cha Kanuni za Nidhamu TFF.