Jumatano , 23rd Mei , 2018

Kocha mkuu wa timu ya Mbao, Novatus Fulgence, amedai kuwa kukosekana kwa mshambuliaji wake tegemezi  Habib Kiyombo ambaye ni majeruhi ndiyo ilikuwa sababu kubwa iliyopelekea timu yake kupoteza mchezo dhidi ya Yanga.

Kocha huyo amesema hayo Mei 22, 2018 wakati akiongea na waandishi wa habari baaada ya kumalizika mchezo huo na kuongeza kuwa Habib Kiyombo ni mchezaji muhimu na ndiye mfungaji bora katika timu ya Mbao kwahiyo kukosekana kwake kumechangia timu hiyo kupoteza mchezo huo.

“Umuhimu wa Habib Kiyombo upo katika timu na ukizingatia yeye ndiye mfungaji bora katika timu yetu, kwahiyo kukosekana kwake kumepunguza kwa kiasi fulani asilimia za kushinda, lakini kingine ukiangalia katika mchezo wa kwanza yeye ndiye alitufungia magoli kwahiyo kutokuwepo kwake kumechangia sisi kupoteza nafasi za wazi ambazo tulizipata” amesema Fulgence 

Kocha Fulgence ameongeza kuwa alijaribu kutumia wachezaji wengi wa kikosi cha pili katika mchezo huo lengo likiwa ni kuwapa uzoefu kwaajili ya maandalizi ya msimu wa ujao wa ligi na kutaka kuonesha ubora wa wachezaji hao ingawa walikuwa hawapati nafasi mara kwa mara.

Jana Mei 22, 2018, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, timu ya Yanga ilishinda bao 1-0 katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam, goli pekee lilifungwa na kiungo Thabani Kamusoko kwa mpira wa adhabu katika dakika ya 26 na hivyo kuifanya klabu hiyo kufikisha alama 51 na kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi.