Ijumaa , 18th Sep , 2020

Raundi ya tatu ya Ligi kuu ya Tanzania Bara itaunguruma mwisho wa wiki hii kuanzia tarehe kumi na tisa siku ya Ijumaa ambapo leo Viwanja viwili vitashuhigiwa Timu nne zikitupa karata zao kusaka alama tatu muhimu.

Salum Aboubakar(Sureboy) wa Azam (Kulia ) na Feisal Salum wa Yanga (Kushoto) katika kipute cha VPL.

SOKOINE -MBEYA

Ihefu ambao ni wageni katika ligi watakua katika Uwanja wao wa nyumbani kwa mara ya tatu mfululizo .

Kikosi cha Ihefu ambacho kinanolewa na Kocha Maka Mwalwisi, kilifungua dimba dhidi ya Mabingwa watetezi Simba,na walipoteza kwa bao 2-1, kabla ya kuinyuka Ruvu Shooting bao 1-0.

Hadi sasa Ihefu wapo nafasi ya 7 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 3,na watakabiliana na Mtibwa Sugar ambao wanawania ushindi wa kwanza msimu huu baada ya kuambulia alama 2 katika mechi 2 walizocheza dhidi ya Ruvu Shooting waliyotoka suluhu na sare ya bao 1-1 na Simba.

USHIRIKA-KILIMANJARO

Polisi Tanzania wao watacheza mechi yao ya kwanza katika Uwanja wao wa nyumbani baada ya kucheza mechi 2 ugenini dhidi ya Azam Fc waliyopoteza kwa bao 1-0 kabla ya kuiduwaza Namungo nyumbani kwao kwa kuwanyuka bao 1-0.

Wakiwa nafasi ya 8 na alama zao 3,Polisi ambayo inanolewa na Kocha Malale Hamsini,watakabiliana na JKT Tanzania ambao katika mchezo uliopita walikubali kipigo cha bao 2-0 kutoka kwa Dodoma Jiji .

Kocha Mohamed Abdallah Baresi wa JKT Tanzania atashuka dimbani leo akiwa na hazina ya alama 3 alizozivuna ugenini katika mechi ya ufunguzi walipoifunga Kagera Sugar bao 1-0 huko Kaitaba.

JKT Tanzania wanakamata nafasi ya 10 katika msimamo wakiwa wamekusanya alama 3 katika mechi 2 walizocheza.