Ijumaa , 20th Apr , 2018

"Baada ya kufanya mazungumzo na kuangalia maslahi ya klabu kwa uangalifu mkubwa na kufanya majadiliano na uongozi wa timu, nimeona ni wakati mzuri kwangu kuachia ngazi mwisho wa msimu huu''.

Huo ni ujumbe wa kocha wa Arsenal, mzee Arsene Wenger ambao ameutoa mapema leo ikiwa ni kuthibitisha kuwa ataachana na timu hiyo baada ya kuifundisha kwa miaka 22.

Wenger mwenye miaka 68 alianza kuifundisha Arsenal Oktoba 1, 1996 na amefanikiwa kuipa mafanikio mengi tofauti tofauti ikiwemo ile rekodi ya kutwaa ubingwa wa EPL bila kufungwa mwaka 2003. Mafanikio ya Wenger ndani ya Arsenal ni kutwaa ubingwa wa EPL mara tatu na Ubingwa wa FA mara saba.

Wenger ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu anaweza kuondoka akiwa ametwaa ubingwa wa Europa League ambapo yupo nusu fainali na atacheza na Ateltico Madrid.

Wenger amewashukuru mashabiki wa Arsenal na kuwataka kuendeleza umoja wao na kuiunga mkono timu ili iweze kuendelea kufanya vizuri huku akiahidi mchango wake wa mawazo ataendelea kuutoa kwa klabu muda wote.