Jumanne , 16th Oct , 2018

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Oktoba 16, 2018 na kusomewa mashtaka mawili na baadaye kuachiwa huru kwa dhamana.

Hans Poppe kulia akiingia kwenye mahakama ya Kisutu.

Hans poppe ameunganishwa katika kesi ya kughushi nyaraka za klabu na utakatishaji wa fedha inayomkabili Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu.

Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro amewasomea washtakiwa wote mashtaka 10 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Katika mashtaka hayo 10 yanayowakabili viongozi hao, Hans Poppe anakabiliwa na mashtaka mawili, shitaka moja ni la kuwasilisha nyaraka za uongo na shitaka lingine ni la kughushi nyaraka ambayo kwa mujibu wa sheria mtuhumiwa anapata dhamana.

Inadaiwa kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016, Aveva, Kaburu na Hans Poppe waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya dola za Kimarekani 40,577 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 90 za Kitanzania.

Baada ya kusomewa mashtaka yao mahakama ilitoa masharti ya dhamana kwa Hans Poppe yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya shilingi milioni 15 kila mmoja masharti ambayo ameyatimiza na kupewa dhamana.

Kwa upande wa Aveva na Kaburu wamerudishwa rumande kwasababu mashtaka dhidi yao hayana dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 19.