Ijumaa , 11th Jun , 2021

Michezo ya nusu fainali ya kikanda ya ligi ya kikapu nchini Marekani 'NBA' imeendelea usiku wa kuamkia leo kwa michezo miwili, Milwaukee Bucks imeisimamisha Brooklyn Nets kwa kupata ushindi wa alama 86-83 huku Utah Jazz wakipata ushindi wa alama 117-111 dhidi ya LA Clippers.

Giannis Antetokounmpo akifunga kwenye mchezo wa usiku wa kuamkia leo dhidi ya Brooklyn Nets.

Ushindi wa Bucks umechagizwa na kiwango bora alichoonesha nyota wake Khris Middleton aliyeibuka nyota wa mchezo kwa kujikusanyia alama 35, rebaundi 15 na assisti 1 na kumpiku mkali wa Nets, Kevin Durrant aliyeambulia alama 30, rebaundi 11 na assisti 5 na '3-point made' 3.

Baada ya kupiga kufunga mtupo mmoja nje ya eneo la D la mpinzani na kuambulia alama tatu (3-point made) mara nane na kufanikiwa kufunga mara 3, Durrant ameendelea kuingia kwenye vitabu vya rekodi kwani amefikisha mitupo hiyo mara 325 na kushika nafasi ya 6 kwenye historia ya NBA

Nae MVP wa misimu miwili iliyopita, Giannis Antetokounmpo wa Bucks aliisaidia timu yake kupata ushindi wa kuweka hai matumaini yao ya kushindania kufuzu fainali baada ya kufungwa michezo miwili ya mwanzo, akipata alama 33, rebaundi 14 na assisti 2.

Kyrie Irving wa Nets aliyecheza bila mlinzi pacha wake James Harden anayesumbuliwa na maumivu ya misuli, aliijikusanyia alama 22, rebaundi 5 na assisti 1 ambazo hazikutosha kuwafanya Nets kuendeleza ubabe wao hivyo watajipanga upya watakapokutana tena siku chache zijazo.

Atakayekuwa wa kwanza kupata ushindi kwenye michezo yake minne ya mwanzo kabla ya mwenzake kwenye mizunguko ya michezo 7 wanayowania basi atatinga fainali kwa ukanda wa Magharibi.

Kwa upande mwingine:

Timu ya Utah Jazz imefanikiwa kuwafunga Los Angeles Clippers kwa alama 117-111 na kupata ushindi wa pili mfululizo kwenye hatua ya michezo hiyo ya nusu fainali kwa ukanda wa Mashariki na kujiwekea mazingira mazuri ya kutinga fainali.

Ni Donovan Mitchell aliyeibeba mabegani Utah kwa kuibuka nyota wa mchezo kwa kukusanya jumla ya alama 37, rebaundi 3 na assisti 4 liha ya kupata upinzani mkali kutoka kwa Jackson Reggie wa Los Angeles Clippers aliyepata alama 29, reabundi 2 na assisti 2.

Paul George alijikusanyia alama 27, rebaundi 10 na assisti 6 na  Kawhi Leonard aliyepata alama 21, rebaundi 4 na assisti 5 ambazo kwa pamoja hazikutosha kuibeba Los Angeles Clippers kupata matokeo mazuri.

Michezo ya nusu fainali za kikanda za NBA zitakazoendelea usiku wa kuamkia kesho ni miwili, Atalanta Hawks dhidi ya Philadelphia 76ers saa nane na nusu usiku ilhali Denver Nuggets watakipiga na Phoenix Suns saa 11 Alfajiri.