Mkude kutojiunga kambini Stars, kocha azungumza

Jumanne , 17th Mar , 2020

Kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinaendelea na mazoezi Jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya AFCON dhidi ya Tunisia na michuano ya CHAN nchini Cameroon.

Jonas Mkude

Jumla ya wachezaji 35 waliitwa kujiunga na Taifa Stars katika mchezo huo na wachezaji wengi wamewasiri kambini isipokuwa wachezaji wa Yanga pamoja na kiungo wa klabu ya Simba, Jonas Mkude ambaye hakuna taarifa rasmi ya kwanini hajajiunga na kambi.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amesema kuwa hana taarifa rasmi kwanini mchezaji huyo hajawasiri kambini na yeye anasubiri taarifa kujua alikuwa wapi.

"Wachezaji ambao hawajafika ni wengi sio Jonas Mkude peke yake, wapo wa Yanga pamoja na wengine wanafika leo jioni lakini Jonas tatizo ni kwamba wachezaji wenzake wamefika yeye hajafika", amesema Ndayiragije.

"Alisema anakwenda Morogoro lakini hatujawa na uhakika aliko pamoja na sababu za kwanini hajafika, lakini kuna msemaji na wale wanaohusika watawapa taarifa. Mimi siwezi kuliongelea jambo ambalo sijalijua vizuri", ameongeza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF, mchezo huo wa kuwania kufuzu AFCON kati ya Taifa Stars dhidi ya Tunisia umeahirishwa kutokana na tishio la virusi vya Corona huku pia michuano ya CHAN iliyotakiwa kufanyika nchini Cameroon kuanzia Aprili 4 -25, imeahirishwa.