Jumanne , 11th Dec , 2018

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo amesema kuwa amethibitishiwa na makamanda wa polisi wa mikoa ya Pwani na Morogoro pamoja na kamanda wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuwa wizi wa vifaa kwenye ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) wataudhibiti.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani (katikati) aliyevaa Glovu.

Akiongea leo mkoani Pwani Mhandisi Ndikilo ameataka makanda hao wahakikishe vifaa haviibiwi kwani mradi huo ni muhimu kwa taifa hivyo lazima ulindwe kwa nguvu yoyote na vyombo dola.

''Hatuwezi kuvumilia kuona vifaa kama Saruji, Nondo na Mafuta ya dizeli, vikiendelea kuibiwa kwenye ujenzi wa mradi wakati vyombo vya usalama vipo ni lazima tuhakikishe vifaa viko salama'', amesema Ndikilo.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wankyo Nyigesa kwa kushirikiana na mwenzake wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema watahakikisha wizi katika maeneo ya Soga, Ngerengere na Morogoro unadhibitiwa.

''Tumeshaanza zoezi la kukamata wezi wa vifaa na tunaendelea hivyo kwa wale ambao hawataki wataendelea kuishia jela'', amesema RPC Wankyo Nyigesa.