Jumamosi , 27th Jul , 2019

Mfanyabiashara Mohammed Dewji amesema haondoki Simba na tayari wameshaongea na serikali na kwamba maendeleo ya mpango wa uwekezaji kwenye klabu hiyo unaendelea vizuri.

Mo Dewji ambaye kwasasa anatambulika kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba amesema amesikitishwa na baadhi ya mambo yanayoendelea mtandaoni ikiwemo kusema Waziri wa Michezo Harrison Mwakyembe ameanzisha utaratibu mpya.

''Nimesikitishwa na mijadala mitandaoni ya kumshutumu Waziri Mwakyembe kwamba ameanzisha utaratibu mpya wa mwekezaji kuwa na 49% na wanachama 51% ya hisa. Ndugu zangu, si kweli. Utaratibu huu upo tangu 2017 kisheria na sisi Simba tulikubali'', ameandika.

Aidha Mo Dewji amesisitiza kuwa, ''Waziri Mwakyembe alituruhusu SIMBA tuendelee na mwekezaji mmoja. Ndugu WanaSimba Mimi nipo na niko na nyinyi, siendi popote. Na sasa tumeishazungumza na Serekali na mazungumzo ni mazuri.

Mbali na hilo mfanyabiashara huyo na mpenzi wa mpira wa miguu hapa nchini amewasihi mashabiki wa Simba kujitokeza kushangilia taifa Stars kwenye mechi ya kesho kuwania kufuzu CHAN 2020 dhidi ya Kenya.

''Nawasihi WanaSimba wote twendeni tukaishangilie Timu ya Taifa na tukutane Simba Day tarehe 6. Tulianza vizuri na Serikali na tutamaliza vizuri na Serikali''.