Ijumaa , 5th Apr , 2019

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji amesema kuwa klabu hiyo itashindana na timu kubwa barani Afrika msimu ujao katika dirisha la usajili.

Mohamed Dewji

Akizungumza na wanahabari kuelekea mchezo wa robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe Jumamosi hii, Mo Dewji amesema kuwa bajeti ya klabu hiyo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku huku kutokana na kukamilika kwa mabadiliko ya mfumo wa kiuendeshaji na kupanuka kwa vyanzo vya mapato ya klabu.

"Mwaka juzi ukilinganisha na mwaka jana, bajeti yetu imekuwa ikizidi kwa asilimia 60 hadi 70 na mwaka huu bajeti unazidi. Kwakuwa mabadiliko yamefanyika vizuri, tumeanza kupata vyanzo vingi vya mapato", amesema Mo.

"Kiujumla tumejitayarisha kushindana na hizi klabu kubwa na kusajili wachezaji wazuri. Tayari kuna kamati maalum ambayo inalifanyia kazi suala la usajili, kuna wachezaji wengi mikataba yao inaisha. Wengi tutaendelea nao na wengine tutawaacha. Kwahiyo tutakuwepo kwenye dirisha la usajili, Afrika ijue kuwa Simba pia itashindana nao kupata saini za wachezaji wazuri ndani ya bara hili".

Pia Mo Dewji amesema kuwa suala la wachezaji Meddie Kagere na Clatous Chama kuendelea kuhudumu Simba msimu ujao liko kwa mwalimu kwa sababu bado wana mkataba na Simba, huku akisisitiza kuwa anamwachia mwalimu kuamua kama ataendelea nao ama la.

Simba itacheza na TP Mazembe Jumamosi, April 6 katika Uwanja wa Taifa, huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 2-1 ilipocheza mara ya mwisho na timu hiyo katika Uwanja wa Taifa msimu wa 2011/2012.

Bonyeza hapa chini kutazama zaidi.