Jumamosi , 16th Feb , 2019

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya klabu ya soka ya Simba Mohammed Dewji, amesema Simba imeshinda mchezo wa leo kwasababu ni timu bora huku mshindi wa tuzo mhamasishaji bora wa mashabiki wa Simba mtandaoni mwaka 2018, Mwana FA akishangaa.

Mwana FA na Mo Dewji

Mwana FA ameonesha kushangazwa na idadi ndogo ya mabao waliyofunga Simba tofauti na matarajio yake. ''Tufunge waarabu wenye kikosi cha bilioni 80 tuwashindwe hawa wenye cha elfu 60?? hamna hiyo‬..kwanza imekuwaje tumewafunga 1 ??'' ameandika Mwana FA.

Kwa upande wake Mo Dewji yeye ameshukuru na kusema walistahili kushinda kwasababu ni timu bora. ''Alhamdulilah! Timu bora imeshinda''.

Kwa upande mwingine mbunge mdogo zaidi Halima Bulembo naye ameonesha kuguswa na matokeo ya mchezo huo huku akishangilia kwa kumpongeza Haji Manara anavyojidai na timu yake. ''Sema Haji Unajuwa Kujishaua Jamani''

Naye Mbunge wa Mikumi Joseph Haule amesema hizi ni salamu tu lakini wanaisubiri AS Vital Club ya DR Congo ili walipe kisasi. ''Leo tumewabeep tu maana nyinyi sio Level yetu, Sasa tunawasubiri wale Wacongo wenu waliowatuma muimbe sana Bolingo wakati ule'', ameandika.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Dar es salaam amewatania viongozi wenzake, Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro na mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Hapi kuwa wanashabikia Yanga kwa heshima ya wazazi wao bila hivyo wangekuwa wameshahama.