Jumanne , 25th Sep , 2018

Ufalme wa mafanikio ya soka duniani wa nyota Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ulisimamishwa kwa mara ya kwanza hapo jana tangu mwaka 2008 baada ya kijana raia wa Croatia, Luka Modric kushinda kwa mara ya kwanza katika historia yake ya soka.

Luka Modric.

Luka Modric alizaliwa 9, Septemba 1985 katika kitongoji cha Modrici, kijiji cha Zaton Obrovacki kinachopatikana katika miteremko ya milima ya Velebit kaskazini mwa jiji la Zadar nchini Croatia ambayo zamani ilijulikana kama Jamhuri ya Yugoslavia. Akiwa na umri wa miaka mitano, Modric alikuwa akichunga mifugo ya familia yake kabla ya kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1991 vilivyopelekea Croatia kupata uhuru wake  na kujitenga kutoka Yugoslavia.

Vita hivyo vilisababisha Luka Modric na babu yake ambaye alikuwa akiishi naye utotoni kulazimishwa kuhama katika kijiji chao kabla ya babu yake kuuwawa na askari na nyumba yao kuchomwa moto kulikopelekea Modric na familia yake kuwa wakimbizi kwa muda wa miaka saba. Baba yake alijiunga na jeshi la Croatia kama fundi na njia pekee ambayo ilimsaidia Modric kuachana na maisha hayo ni kupitia soka, mwenyewe anakiri kuwa maisha hayo magumu ya utotoni ndiyo yaliyomtengeneza kuwa mtu mwema anayeonekana hivi sasa.

Katika maisha hayo ya ukimbizi, Modric akisaidiwa na wazazi wake alihudhuria katika vituo mbalimbali vya soka hadi alipofanikiwa kujiunga na klabu ya Dynamo Zagreb mwaka 2001 akiwa na umri wa miaka 16. Alisaini mkataba mrefu na klabu hiyo msimu wa 2005/06 na pesa yake ya kwanza aliyoipata kupitia mkataba wake aliwanunulia nyumba wazazi wake katika mji wa Zadar.

Aliondoka Dynamo Zagreb msimu wa 2008/09 na kujiunga na Tottenham Hortspurs akiwa ameifungia klabu hiyo mabao 26 na 'Assists' 29 katika michezo 94 na kuisaidia klabu yake kushinda kombe la ligi nchini Croatia.

Alicheza Tottenham Hortspurs kwa mafanikio makubwa na kuisaidia klabu hiyo kuwa moja ya klabu bora na yenye ushindani katika ligi kuu nchini Uingereza, aliondoka Spurs na kujiunga na Real Madrid mwaka 2012 akiwa ameichezea jumla ya michezo 127 na kufunga mabao 13.

Msimu wa kwanza akiwa Real Madrid hakufanya vizuri na alitajwa kuwa ni moja katia ya usajili mbovu katika klabu hiyo, lakini juhudi na ufundi wake ulimsaidia kupata nafasi ya kikosi cha kwanza ambapo mpaka sasa ameisaidia klabu yake kushinda jumla ya mataji 14, yakiwemo Laliga, Copa del Rey, klabu bingwa Ulaya(4), UEFA Super Cup(3), klabu bingwa dunia(3).

Mwaka huu umekuwa ni wa mafanikio makubwa kwake ambapo ameweza kushinda tuzo kubwa tatu mpaka sasa, mchezaji bora wa michuano ya kombe la dunia, mchezaji bora wa Ulaya na mchezaji bora wa dunia wa FIFA. Amewashukuru mashabiki na wadau wa soka kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kusema,

"Naielekeza (tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa FIFA) kwa kila mmoja anayependa soka"