Jumatatu , 24th Sep , 2018

Tarehe ya ugawaji wa tuzo mbalimbali kwa wachezaji na makocha za shirikisho la soka duniani FIFA, maarufu kama 'FIFA Best Awards' imewadia ambapo tukio hilo litafanyika usiku wa hii leo jijini London nchini Uingereza.

Tuzo hizo zinafanyika kwa mara ya tatu hivi sasa baada ya FIFA kujitoa katika ushirikiano na tuzo za Ballon d'Or za Ufaransa ambazo walishirikiana tangu mwaka 2010 hadi 2016.

Kipengele kikubwa kinachovuta hisia za watu katika usiku huu wa leo ni kile cha mchezaji bora wa dunia kwa upande wa wanaume ambacho kinawaniwa na kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric, Mohamed Salah wa Liverpool na Cristiano Ronaldo anayekipiga katika klabu ya Juventus.

Luka Modric ambaye aliwahi kucheza katika klabu ya Tottenham Horspurs kabla ya kujiunga na Real Madrid, anarejea tena nchini Uingereza huku akipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi wa tuzo hiyo kutokana na mafanikio mbalimbali aliyoyapata katikati ya mwaka uliopita na mwaka huu.

Mafanikio aliyoyapata Luka Modric katika kipindi hicho ni kushinda klabu bingwa Ulaya, ubingwa wa 'European Super Cup',  kucheza fainali ya kombe la dunia na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa michuano hiyo pamoja na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya. Wadau wengi wa soka wanaamini mafanikio hayo ndiyo yatakayompa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi wa tuzo hiyo.

Cristiano Ronaldo alimaliza msimu uliopita kwa kufunga idadi ya mabao 44 katika mashindano yote huku akiibuka mfungaji bora wa michuano ya klabu bingwa Ulaya na kuisaidia Real Madrid kushinda taji hilo. Hakufanya vizuri katika michuano ya kombe la dunia na pia hakufanikiwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya licha ya kuwa katika kipengele kimoja na Modric lakini anapewa nafasi ya kuibuka na tuzo hiyo kutokana na mafanikio akipokuwa na Real Madrid msimu uliopita.

Kwa upande wa Mohamed Salah, wengi miongoni wa wadau wa soka wanaamini mchezaji huyo hakustahili kuwepo katika listi ya wachezaji hao watatu wa mwisho, lakini ni wazi kuwa kiwango chake kizuri hasa msimu uliopita ndicho kilichompa nafasi ya kuwepo katika listi hiyo. Alifunga mabao 44 katika michuano yote, aliisaidia Liverpool kucheza fainali ya klabu bingwa Ulaya, alishinda tuzo ya mfungaji na mchezaji bora wa EPL pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa Afrika japo hakufanya vizuri katika michuano ya kombe la dunia, timu yake ya taifa ya Misri ikitolewa hatua ya makundi.

Mashabiki ndiyo watakaoamua ni nani mshindi wa tuzo hiyo usiku wa leo kupitia kura zao walizopiga katika tovuti ya FIFA tangu mwezi uliopita. Tuzo zingine zitakazotolewa ni pamoja na kocha bora wa mwaka, goli bora na kikosi bora cha mwaka cha FIFA ambapo tuzo hizo zote zitatolewa katika pande zote mbili, soka la wanawake na wanaume.