Jumatatu , 27th Jul , 2020

Mfanyabiashara na Mwekezaji wa Klabu ya Simba Mohammed Dewji "Moo Dewji", amemuomba Rais John Pombe Magufuli kubadili jina la Uwanja wa Taifa kuwa Uwanja wa Benjamin William Mkapa.

Mfanyabiashara na Mwekezaji wa Klabu ya Simba Moo Dewji na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa

Moo Dewji ameomba  hilo kupitia mtandao wa Instagram huku akiweka sababu 8 za kutaka uwanja huo kubadilishwa kuwa Uwanja wa Mkapa na kutaka Watanzania wengine waunge mkono bila ya kujali ushabiki, hizi ni baadhi ya sababu alizozitaja Moo Dewji ili kubadilishwa jina la uwanja huo,

"Ujenzi wa Uwanja wa Taifa wa Jijini Dar es Salaam, ulianzishwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, Uwanja huo wenye uwezo wa kubeba mashabiki 60,000 ni miongoni mwa viwanja bora katika Bara la Afrika kwa sasa".

"Uwanja huo kwa namna mmoja au nyingine umesaidia kuendeleza mpira wa miguu na michezo mingine nchini Tanzania, uzuri na ukubwa wa soka letu umedhihirishwa kwa sababu ya uwanja wetu huo ambao unashika nafasi ya 11 kwa ukubwa Afrika".

"Nje ya michezo, mashindano ya usomaji wa Quran yaliona mkusanyiko mkubwa zaidi kwenye mashindano makubwa ya kusoma Quran Barani Afrika, hii nayo ilikuwa ni rekodi nzuri kwetu Watanzania".

"Tumeshuhudia matamasha mbalimbali makubwa kama matamasha ya Pasaka na Krismasi yakifanyika hapo na lengo la yote hayo ni kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania"

"Itakuwa ni heshima kubwa kama uwanja wetu pendwa utaitwa jina la Uwanja wa Benjamin William Mkapa, tunamuomba Rais John Pombe Magufuli aridhie kubadili jina la uwanja huo kwa heshima ya Hayati Mkapa ili tuendelee kumkumbuka kwa mchango wake mkubwa na hasa kwa vizazi vijavyo" ameandika Moo Dewji.