Morrison ataka kuwachanganya mashabiki wa Yanga

Ijumaa , 20th Mar , 2020

Nyota maarufu ndani ya klabu ya Yanga hivi sasa, Bernard Morrison amesema kuwa ana vitu vingi vya kufanya kwa mashabiki wa klabu hiyo ili kuwapa kile kitu wanachokitaka.

Bernard Morrison

Amesema hayo kufuatia sapoti kubwa ambayo amekuwa akioneshwa na mashabiki wa Yanga tangu alipojiunga na nayo katika dirisha dogo la usajili mwezi Januari.

Morrison amesema kuwa alipokuwa akicheza soka nchini Congo DR na Afrika Kusini amejifunza vitu vingi ambavyo akivifanya, mashabiki watampenda kwa kiwango kikubwa zaidi na kwamba baada ya muda atavionesha vitu hivyo.

"Nilipokuwa Orlando Pirates ya Afrika Kusini nilijifunza vitu vingi sana kutoka kwa wachezaji wenzangu hasa kuhusu mitindo ya uchezaji na nafikiri nina vingi vya kuonesha lakini kwanza kwa sasa nataka kufunga magoli", amesema.

"Najua wanapenda ninavyofanya na mimi nataka nifanye zaidi kwa ajili yao kwa sababu wanakuja nyumbani kufurahia", ameongeza.

Kuhusu tetesi za kuhusishwa na klabu ya Simba, Morrison amesema kuwa yeye hana anachokifahamu kuhusu hilo kwani kwa sasa yupo na mkataba katika klabu ya Yanga, huku akiwashukuru amashabiki wengi ambao wamekuwa wakijitokeza kila mechi anazocheza kumpa zawadi mbalimbali.