Ijumaa , 24th Jan , 2020

Mshambuliaji mpya wa klabu ya Yanga, Bernard Morrison amezungumzia juu ya kiwango chake alichokionesha katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya Singida United.

Bernard Morrison na kocha Luc Eymael

Katika mchezo huo uliofanyika Jumatano, Januari 22 katika Uwanja wa Liti mjini Singida, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 ambapo mabao hayo yalifungwa na David Molinga, Haruna Niyonzima na Yikpe Gislam, Morrison alionesha kiwango kikubwa ikiwemo kuhusika katika mabao mawili na kuwakosha mashabiki muda wote ambao aliocheza.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Morrison amesema kuwa kiwango alichokionesha ni cha kawaida kwake kwani soka la maeneo mengi aliyopitia halitofautiani.

"Tumekuja huku tukiwa na lengo la kushinda mechi, ni furaka kwetu kwa ushindi tulioupata ambao umerejesha hali ya kujiamini na furaha miongoni mwetu", amesema Morrison.

"Popote unapopata nafasi ya kuonesha uwezo wako ni vyema kuitumia vizuri ili kuleta matokeo ya ushindi ambayo mashabiki na benchi la ufundi watayafurahia", ameongeza.

Baada ya mchezo huo, Yanga inerejea Jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa kombe la shirikisho dhidi ya Tanzania Prisons.