Jumatano , 20th Nov , 2019

Tottenham Hotspur imemtangaza Jose Mourinho kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu utakaomalizika mwishoni mwa msimu wa 2022/23.

Jose Mourinho

Uteuzi huo wa Mourinho umekuja ndani ya masaa 24 tangu kufutwa kazi kwa aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo Mauricio Pochettino.

Jana usiku Tottenham ilieleza kuwa pande mbili zimefikia makubaliano ya kuvunja mkataba pamoja na wasaidizi wote wa Pochettino, ambao ni Jesus Perez, Miguel D’Agostino na Antoni Jimenez.

Mourinho ambaye hakuwa na timu tangu msimu uliopita alipofukuzwa Manchester United alianza kutajwa kuchukua nafasi hiyo mara tu baada ya Spurs kutangaza uamuzi wake huo.

Mwenyekiti wa Tottenham Daniel Levy amesema uwepo wa Mourinho unawapa uhakika wa kufanya vizuri kwasababu ni miongoni mwa makocha bora duniani.

Kwa upande wake Mourinho amesema amefurahia nafasi yake hiyo mpya kutokana na ubora wa kikosi cha Tottenham kuanzia timu kubwa mpaka timu za vijana, hivyo ana shauku kubwa ya kufanya kazi na timu ya aina ile.