Alhamisi , 4th Apr , 2019

Mshambuliaji wa TP Mazembe, Tresor Mputu amezua balaa miongoni mwa mashabiki wa klabu hiyo waliojitokeza kuipokea timu yao katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.

Tresor Mputu akiongea na wanahabari

TP mazembe walitua katika Uwanja wa Ndege wa Songwe kabla ya kuwasili Dar es salaam, ambapo imeelezwa kuwa walitua kwaajili ya kufanya matengenezo madogo.

Baada ya kutua Dar es salaam, wachezaji na viongozi walipokelewa na mashabiki wao waliojitokeza, ambao muda wote walikuwa wakiimba nyimbo za Kikongo na Kifaransa. Shangwe lao liliongezeka zaidi baada ya kumuona mshambuliaji hatari wa klabu hiyo, Tresor Mputu ambaye ana mabao manne mpaka sasa katika Klabu Bingwa Afrika.

Inaelezwa kuwa baada ya kutua, Mazembe waligomea basi kubwa lililoandaliwa na wenyeji klabu ya Simba, bali walitumia mabasi madogo mawili na basi waliloandaliwa lilitumiwa na mashabiki wao.

Wakati huo huo wenyeji wa mchezo, klabu ya Simba wameianza safari asubuhi ya leo kurejea Dar es salaam kutoka mjini Morogoro, kufuatia mchezo wao kuahirishwa Jumatano, April 3 baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha uwanja wa Jamhuri kujaa maji.

Mchezo huo wa Klabu Bingwa Afrika baina ya Simba na TP Mazembe utapigwa Jumamosi, April 6 katika Uwanja wa Taifa saa 10 jioni.