Alhamisi , 17th Jun , 2021

Klabu ya Real Madrid imethibitisha kuwa itaachana na nahodha wake Sergio Ramos pindi mkataba wake na klabu hiyo utakapo malizika mwishoni mwa mwezi huu, baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka 16.

Sergio Ramos

Ramos anaondoka Madrid baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya, ambapo Ramos alikuwa anahihitaji mkataba wa miaka miwili na ongezeko la mshahara, wakati klabu ilimpa ofa ya mkataba wa mwaka mmoja na punguzo la asilimia 10 kutoka kwenye mshahara wake wa sasa, hivyo wakafikia muafaka wa kutosaini mkataba mpya kutokana na kutofautiana kwenye vipengele hivyo.

Mlinzi huyo wa kati mwenye umri wa miaka 35 alijiunga na Madrid mwaka 2005 akitokea Sevilla na ameshinda jumla ya mataji 22 akiwa na Los Blancos ambapo ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu La Liga mara 5 na ubingwa wa klabu bingwa ulaya mara 4.

Msimu wa 2020-21 haukuwa mzuri kwa Ramos kwani aliandamwa na majeruhi ya mara kwa mara ambayo yamemsababishia kutojumuhishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania kinachoshiriki michuano ya Euro 2020 inayoendelea. Ndani ya msimu huo alicheza michezo 21 ikiwa ni idadi ndogo zaidi tangu ajiunge na klabu hiyo.

Vilabu vya PSG ya Ufaransa na klabu yake ya zamani ya Sevilla ndio vinatajwa kuonyesha nia ya kuhitaji huduma ya Ramos.