Namungo FC wazidi kuchafua hali ya hewa

Alhamisi , 6th Jun , 2019

Msimu timu mbalimbali zinaendelea kujiandaa na usajili kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara, Namungo FC imeendelea kutikisa katika usajili.

Usajili wa Namungo FC

Namungo FC yenye makao yake makuu wilayani Ruangwa mkoani Lindi imeendelea kutikisa katika usajili, ambapo hadi sasa imesajili wachezaji wanne watakaoitumikia timu hiyo msimu ujao.

Mchezaji wa kwanza ambaye imemsajili ni Bigirimana Blaize kutoka Alliance FC, ambapo amesaini mkataba wa mwaka mmoja. Mwingine ni Daniel Joram ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu hiyo. Joram aliitumikia Namungo FC kwa mkopo msimu uliopita akitokea Mbeya City.

Pia Namungo FC imeimarisha mikataba ya wachezaji wake wawili, mlinzi, Jukumu Kibanda pamoja na mshambuliaji Lusajo Reliants kwa mkataba wa miaka miwili. 

Kutokana na usajili wanaoufanya Namungo FC, kuna kila dalili ya timu hiyo kufanya vizuri msimu ujao kama ilivyokuwa kwa klabu ya KMC katika msimu wake wa kwanza uliomalizika, ambapo imemaliza nafasi ya nne ya msimamo na kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.