Ijumaa , 18th Oct , 2019

Kaimu kocha mkuu wa timu ya Taifa ya soka ya Tanzania, Etienne Ndayiragije amesema timu yake imefanikiwa kujiandaa vizuri, licha ya kupitia changamoto ya kupata uwanja wa mazoezi nchini Sudan.

Kaimu kocha mkuu wa timu ya Taifa ya soka ya Tanzania, Etienne Ndayiragije

Ndayiragije ameyasema hayo kuelekea mchezo wa leo wa kuwania kufuzu CHAN dhidi ya Sudan ambao utapigwa kwenye uwanja wa Al-Merrikh huko Omdurman.

'Tumefanya maandalizi vizuri kama unavyojua kupata uwanja wa mazoezi ugenini ni changamoto lakini tulikuwa na mpango mbadala na tumefanikiwa, wachezaji wote wapo vizuri na mmoja aliyeumia Rwanda Mohamed Hussein naye anaendelea vizuri', amesema.

Ameongeza kuwa baada ya Mohamed Hussein kuumia wakiwa Rwanda, alimpumzisha kwenye mchezo wa kirafiki uliopigwa Oktoba 14, dhidi ya Rwanda na kuisha kwa suluhu. Lakini kwasasa yupo sawa na anaweza kucheza mchezo wa leo.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Dar es salaam, Sudan walishinda 1-0, hivyo Taifa Stars ina kazi ya kubadilisha matokeo ili iweze kusonga mbele.