Neymar atamani angekuwa na PSG

Jumatatu , 16th Apr , 2018

Nyota wa klabu ya PSG na timu ya taifa ya Brazil Neymar Jr, ameipongeza klabu yake hiyo kwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Ufaransa (Ligue 1) huku akiweka wazi kuwa alitamani sana kuwepo wakati wanatwaa ubingwa.

Neymar hayupo na timu yake tangu mwezi Februari kufuatia kuumia mguu na kulazimika kusafirishwa kwenda nchini kwao Brazil kwaajili ya matibabu ambayo yalitazamiwa kutumia miezi mitatu hadi minne.

Baada ya jana PSG kutwaa ubingwa huo Neymar aliwapongeza wachezaji wenzake kupitia mitandao yake ya kijamii ambapo aliandika ''Nilitamani sana kuwa pamoja na nyie, hongereni kwa ubingwa''.

PSG usiku wa jana waliibuka na ushindi mnono wa mabao 7-1 dhidi ya Mabingwa watetezi Monaco. Baada ya ushindi huo PSG wamefikisha alama 87 ambazo haziwezi kufikiwa na Monaco yenye alama 70 huku zikiwa zimebaki mechi 5 pekee.

Ubingwa huu ni wa 7 kwa PSG ikiwa imetwaa katika misimu ya 1985–86, 1993–94, 2012–13, 2013–14, 2014–15, 2015–16 na 2017–18.