Jumanne , 10th Jan , 2017

Wapenzi na mashabiki wa soka visiwani Zanzibar leo wanataraji kupata burudani ya aina yake kwa kuwashudia watani wa jadi katika soka la Bongo Simba na Yanga wakipambana katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani humo

Wachezaji wa Yanga (juu) na wa Simba (chini)

 

Mchezo huo ambao ni wa pili ukipigwa majira ya saa 2:15 usiku, unataraji kuvuta hisia za wengi huku mamia ya mashabiki wakizidi kumiminika visiwani humo kutoka Tanzania Bara kwa ajili ya kushuhudia mtanange huo.

Yanga inaingia ikiwa na kumbukumbu ya kupigwa mabao 4-0 na Azam katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi huku ikijivunia kutoa kipigo kikubwa zaidi cha mabao 6-0 kwa Jamhuri ya Pemba, huku Simba ikijivunia kumaliza hatua ya makundi bila kupoteza mchezo licha ya kuonesha udhaifu katika safu yake ya ushambuliaji.

Kinachotia hamasa zaidi katika mchezo huo ni kitendo cha timu zote mbili kupeleka vikosi vyake kamili, ambavyo kwa ajili ya kulinda heshima, makocha wote watalazimika kupanga vikosi vyao imara zaidi katika mechi ya leo.

Takwimu zinaonesha kuwa katika mara 4 ambazo timu hizo zimekutana visiwani Zanzibar, Simba imeshinda mechi 3 huku Yanga ikishinda mechi 1 pekee, jambo ambalo linampa imani Msemaji wa Simba, Haji Manara ambaye amesema Simba ni lazima ishinde kutokana na kuwa na kikosi bora kuliko Yanga.

Mechi ya mwisho kwa Simba na Yanga kukutana visiwani humo na Simba kushinda 2-0

Kwa upande wa Yanga, wapenzi na mashabiki zake wametoa tambo kuwa ni lazima mnyama achinjwe kwa kuwa Simba haina kitu, na haina kikosi imara kama cha Yanga, huku wakijipa moyo kuwa kufungwa na Azam ilikuwa ni njia ya kutafuta hasira za kumuangamiza mnyama na wala hakuwastui.

Mchezo wa mwisho kwa timu hizo kukutana Zanzibar, Simba ilishinda mabao 2-0 kupitia kwa Mgosi na Shija Mkina.

Mchezo mwingine wa nusu fainali, utazikutanisha Azam FC, na Taifa Jang'ombe kuanzia saa 10:00 jioni.

Kikosi cha Azam FC katika mazoezi