''Nimekula sumu ya chakula'' - Manara

Jumatatu , 24th Sep , 2018

Baada ya jana kuumwa ghafla akiwa mkoani Shinyanga, msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara ameweka wazi kuwa haumwi presha wala ugonjwa wa moyo badala yake vipimo vya awali vina viashiria kuwa amepata madhara kutokana na kula chakula kisichofaa.

Haji Manara

Manara ameeleza hilo leo baada ya kutua jijini Dar es salaam, akitokea Shinyanga ambako Simba ilicheza mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Mwadui FC na kushinda mabao 3-1 jana jioni.

Manara alianza kuumwa jana baada ya mchezo wa Simba na Mwadui FC, huku awali ikiripotiwa kuwa ni tatizo la presha kabla ya madaktari wa Shinyanga na baadaye Mwanza kumfanyia vipimo vya awali na kubaini hakuna tatizo la presha.

Mchezo wa Simba jana ulikuwa ni wa pili kwa timu hiyo kucheza kanda ya ziwa msimu huu ambapo ilianzia jijini Mwanza na kupata kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbao FC.