Ijumaa , 10th Aug , 2018

Dirisha la usajili kuelekea msimu mpya wa EPL, 2018/19 limefungwa usiku wa jana huku kila timu ikijiimarisha katika usajili wa wachezaji mbalimbali tayari kwa mchakamchaka wa ligi hiyo unaoanza usiku wa leo.

Jumla ya kiasi cha usajili kwa klabu za EPL kilichotumika ni pauni 1.26 billioni huku vilabu hivyo vikisajili jumla ya wachezaji takribani 121 kutoka vilabu vingine vya ndani na nje ya ligi hiyo.

Klabu ya Liverpool imeongoza kwa kutumia gharama kubwa katika usajili msimu huu, ikitumia jumla ya pauni 155.4 millioni katika usajili wa wachezaji  wanne baada ya kutoa kiasi cha wachezaji waliouzwa, ikifutiwa na Chelsea iliyotumia pauni 87.3 millioni na namba tatu ikifuatiwa na West Ham United.

Rekodi ya kushangaza iliyowekwa katika usajili wa msimu huu ni ya klabu ya Fulham iliyorejea EPL baada ya misimu kadhaa kupita, ikiwa imetumia jumla ya pauni 72 millioni katika kununua wachezaji, rekodi ambayo haijawahi kuwekwa na klabu yoyote katika msimu wake wa kwanza kupanda ligi kuu, ikiwa imenunua wachezaji 12.

Tottenham Hortspurs nayo imeingia kwenye rekodi baada ya dirisha la usajili kufungwa ikiwa haijanunua mchezaji yoyote licha ya kuhusishwa na tetesi kadhaa kipindi dirisha la usajili likiendelea, hiyo ni kutokana na kutumia gharama kubwa katika ujenzi wa uwanja wake mpya ambao watauzindua msimu huu.

Mchezo wa ufunguzi wa EPL leo ni kati ya Manchester United na Leicester City. Kocha wa Man United, Jose Mourinho amethibitisha kuwa atawakosa wachezaji kadhaa katika mchezo huo wakiwemo Nemanja Matic, Diogo Dallot pamoja na mastaa kadhaa ambao wamechelewa kujiunga na timu baada ya likizo zao kumalizika.

Msimu uliopita katika ligi, timu hizo zilikwenda sare mchezo mmoja na mchezo mmoja ulishuhudiwa Man United ikishinda kwa mabao 2-0 katika uwanja wa Old Trafford.