Ijumaa , 23rd Feb , 2018

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino amemwahidi Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa kuwa FIFA itawekeza katika miradi ya maendeleo ya soka nchini.

Infantino ametoa ahadi hiyo jana katika mazungumzo yake maalum na Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa ofisini kwake baada ya kumtembelea ikiwa ni sehemu ya ratiba zake nchini baada ya kumaliza mkutano mkuu wa FIFA wa mwaka wa kikanda.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania inaunga mkono juhudi za FIFA katika kupambana na rushwa kwenye soka pamoja na matumizi mabaya ya fedha na madaraka.

Rais huyo aliyechukua mikoba ya Mswisi Joseph ‘Sepp’ Blatter Februari 26 mwaka 2016 ameunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kupambana na rushwa katika sekta ya michezo.

Aidha Infantino ameishukuru Serikali kwa ukarimu wake na kumuomba Waziri Mkuu Majaaliwa kufikisha salamu za shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa mapokezi mazuri.