Jumatano , 15th Aug , 2018

Mabingwa mara 12 wa ligi ya mabingwa ulaya, Real Madrid wanatarajia kushuka dimbani usiku wa leo dhidi ya mabingwa wa Europa League msimu uliopita, Atletico Madrid katika mchezo wa UEFA Super Cup.

Real Madrid wakishangilia kushinda kombe la UEFA Super Cup, 2017.

Katika mchezo huo ambao utapigwa katika dimba la, A Le Coq Arena nchini Estonia, Real Madrid watausaka ubingwa wa Super Cup kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kufanikiwa kushinda klabu bingwa ulaya kwa mara ya tatu mfululizo pia mwaka uliopita mbele ya Liverpool.

Real Madrid imecheza mchezo wa UEFA Super Cup mara sita na kushinda taji hilo mara nne ikiwemo mwaka 2016 dhidi ya Sevilla na mwaka 2017 dhidi ya Manchester United, huku Atletico Madrid ikicheza michezo miwili ya kombe hilo na kufanikiwa kushinda mara zote walizocheza, mwaka 2010 na 2012.

Klabu hizo zimekutana mara tisa katika michuano ya ulaya, Real Madrid ikishinda mara tano huku Atletico Madrid ikifanikiwa kushinda mara mbili na mara mbili zikitoka sare.

Vikosi vya klabu zote mbili vina mabadiliko makubwa kuelekea mchezo huo, ambapo Real Madrid imewatambulisha wachezaji kadhaa  akiwemo mlinda mlango Thibaut Courtois, Vinicius Jr, Javi Sachez, Raul de Tomas pamoja na kocha mpya, Julen Lopetegui baada ya kuachana na nyota wao Cristiano Ronaldo na  Zinedine Zidane mwishoni mwa msimu uliopita.

Atletico Madrid nao wakiwa na wachezaji kadhaa wapya akiwemo kiungo, Thomas Lemar aliyejiunga na klabu hiyo kwa pauni 58 millioni kutoka AS Monaco, wengine ni mshambuliaji wa Croatia, Nicola Kalinic, Gerson Martins na mlinzi, Santiago Arias, baada ya kuachana na Gabi Fernandez na Fernando Torres.