Jumamosi , 23rd Jun , 2018

Mkurugenzi wa timu ya magari ya Red Bull Christian Horner, ameeleza kuwa pamoja na kuwa mkataba wa dereva kinara wa timu hiyo Daniel Ricciardo, kuelekea mwisho lakini hawategemei kumuona akiondoka licha ya kuhitajiwa na timu zingine.

Dereva Daniel Ricciardo wa timu ya Red Bull

Bosi huyo wa Red Bull ameyasema hayo kufuatia mashabiki wengi wa timu hiyo, kuhoji kuhusu uongozi kushindwa kutoa tamko wakati mkataba wa mkali huyo wa magari unamalizika mwishoni mwa mwaka huu.

''Ricciardo amekuwa dereva mzuri na amefanikiwa akiwa na sisi hivyo tunatarajia kumuona akiwa na sisi kwa muda mrefu zaidi lakini hatuwezi kukataa kuwa kuna ofa nyingi amepokea kutoka McLaren na Renault na zaidi sasa kuna ofa mpya kutoka Mercedes na Ferrari, uamzi ni wake lakini tutashangaa akiondoka'', amesema Horner.

Katika mbio za Formula 1 msimu huu, Ricciardo anashika nafasi ya 4 akiwa na alama 84 huku pia akiwa amefanikiwa kuongoza kwenye mbio za Monaco Grand Prix pamoja na Chinese Grand Prix.

Formula 1 inaendelea kesho ambapo zitafanyika nchini Ufaransa zikifahamika kama 'French Grand Prix'. Baadae leo zitafanyika mbio za kuwania nafasi ya kupanga gari kesho wakati wa mbio hizo.