Jumatano , 9th Jan , 2019

Wapinzani wa Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika kundi D, timu ya JS Saoura ya Algeria wanatarajiwa kutua nchini kesho Alhamis tayari kwa mchezo huo utakaopigwa Jumamosi kwenye uwanja wa taifa Dar es salaam.

Wachezaji wa JS Saoura

Katika mchezo huo, Simba inatakiwa kuutumia vizuri ili kuweza kupata alama 3 muhimu ambazo si rahisi sana kuzipata kwenye mchezo wa marejeano huko mjini Méridja Algeria kutokana na rekodi nzuri ya JS Sauora kwenye uwanja wao wa nyumbani maarufu kama 'August 20, 1955'.

JS Saoura waliweka rekodi ya kucheza mechi 58 kwenye uwanja wao wa nyumbani bila kupoteza hata mchezo mmoja. Mechi hizo zilichezwa kati ya Februari 6, 2015 hadi Septemba 15, 2018.

JS Saoura ambayo ilianzishwa mwaka 2008, ilipanda kucheza ligi kuu ya Algeria msimu wa 2012/13. Msimu wa 2015/16 ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili. Msimu uliopita 2017/18 ilimaliza katika nafasi ya pili pia na kupata tiketi ya kushiriki ligi ya mabingwa Afrika.

Kuelekea mchezo huo wa Jumamosi wachezaji 18 wa kikosi cha kwanza cha Simba wamerejea leo jijini Dar es salaam wakitokea visiwani Zanzibar ambapo walikuwa wakishiriki michuano ya Mapinduzi na tayari wamefuzu nusu fainali.