
Wachezaji wa Arsenal wakishangilia baada ya kushinda Ngao ya Hisani
Ushindi wa taji hilo la ngao ya hisani umeifanya timu hiyo kufikisha taji lao la kumi na sita ambapo wamezidiwa na Manchester United yenye rekodi ya kushinda ngao hiyo mara ishirini na moja.
Alikua ni Pierre-Emerick Aubameyang aliyeiyeifanya timu yake kuongoza katika mchezo huo baada ya kufunga goli dakika ya kumi na mbili ya mchezo kipitia kwa Bukayo Saka.
Aubayang amefunga tena goli kwenye uwanja wa Wembley ikiwa zimepita wiki chache tu tokea afunge goli mbili katika mchezo wa fainali ya FA dhidi ya Chelsea.
Liverpool ilisawazisha bao lililofungwa na mchezaji huyo kupitia kwa mchezaji Takumi Minamino aliyeingia kwenye mchezo huo akitokea benchi.
Arsenal imefanikiwa kuitwaa ngao hiyo ya hisani baada ya wachezaji wake wote kufunga penati zao, huku mchezaji wa Liverpool Rhian Brewster yeye akikosa penati yake iliyogonga mwamba wa juu wa goli.
Hilo linakua taji la pili la Mikael Arteta kocha wa washika bunduki hao tokea akabidhiwe kibarua cha kukinoa kikosi cha Arsenal.
Timu hiyo inategemea kucheza mchezo wake wa kwanza wa ufunguzi wa ligi kuu ya England dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Fulham katika uwanja wa Craven Cottage.