Alhamisi , 16th Aug , 2018

Baada ya Atletico Madrid kufanikiwa kuwazamisha mahasimu wao katika mji wa Madrid, Real Madrid kwa mabao 4-2 usiku wa jana. Huu hapa ni mkusanyiko wa rekodi mbalimbali zilizowekwa katika mchezo huo.

Timu ya Atletico Madrid wakishangilia.

Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone ameweka rekodi ya kipekee katika klabu ya Atletico Madrid baada ya ushindi wa taji la UEFA Super Cup, ikiwa ni msimu wake wa saba tangu ajiunge na klabu hiyo.

Kocha huyo machachari awapo uwanjani, ameweka rekodi ya kuwa kocha mwenye mafanikio kuliko wote waliopita katika klabu hiyo, akiwa ameisimamia timu hiyo jumla ya michezo 382 na michezo 236 kati ya hiyo akishinda na kufanikiwa kushinda makombe saba, ameipiku rekodi ya kocha Luis Aragones aliyeshinda makombe sita.

Rekodi nyingine ya kocha wa Real Madrid, Julen Lopetegui ambaye ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kupoteza mchezo wake wa kwanza wa kimashindano tangu Bernd Schuster alipofanya hivyo mwaka 2007.

Katika mchezo huo pia, Lopetegui ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kufungwa mabao manne au zaidi katika mchezo wake wa kwanza wa mashindano tangu Michael Keeping alipofanya hivyo miaka 60 iliyopita alipofungwa na Celta Vigo.

Tangu mwaka 2009 mpaka 2018 timu kutoka Hispania ndizo zilizotwaa taji la Uefa Super Cup isipokuwa mwaka 2013 ambapo Bayern Munich ndiyo ilitwaa taji hilo, timu hizo za Hispania zimetwaa mara tatu kila moja. Barcelona imetwaa mwaka (2009, 2011, 2015), Atletico Madrid imetwaa mwaka (2010, 2012, 2018) na Real Madrid imetwaa mwaka (2014, 2016, 2017).

Goli la kwanza la Diego Costa nalo limengia katika rekodi ya kuwa goli la mapema zaidi katika historia ya mchezo wa Uefa Super Cup, akitumia sekunde 49 pekee kufunga bao hilo.

Klabu ya Atletico madrid imefikia rekodi ya klabu ya Liverpool ya kutwaa taji hilo mara tatu, ambapo imebeba mwaka 2010 waliifunga Inter Milan, 2012 waliifunga Chelsea na 2018 wameifunga Real madrid.